TUMEJIFUNZA NA TUMEBURUDIKA - SEMINA YA WATUMISHI WA SOMA BIBLIA
Anne Gihlemoen
Mwaka huu wafanyakazi wa Soma Biblia tulipata nafasi ya kukutana kwa pamoja katika kituo cha Mikutano cha Amabilis, mjini Morogoro kuanzia tarehe 23 hadi 27 Mei 2018. Wafanyakazi wa vituo vya Soma Biblia toka Arusha, Dar es salaam, Iringa, Mbeya na Mwanza walihudhuria semina hiyo. Pia tulikuwa na waendesha mada mbalimbali toka Chama cha Biblia Tanzania, na Mchg Oswald Ndelwa kutoka Iringa, ambaye aliendesha somo la Biblia kwa siku mbili.
Moja ya madhumuni ya semina hii ilikuwa kukaa kwa pamoja, na kutathmini juu ya wito wetu wa kuwafikia watu wengi zaidi kwa njia ya kusambaza maandiko mbalimbali. Pia ilikuwa ni fursa nzuri kwa wafanyakazi kukutana, kujadiliana, kubadilishana mawazo na mbinu mbalimbali za kueneza injili kwa njia ya maandiko. Ilikuwa pia ni nafasi nzuri ya kushiriki michezo kwa ajili ya afya zetu, na kutembelea vivutio mbalimbali vya mji wa Morogoro kama vile mbuga za wanyama Mikumi, pamoja na milima ya Uluguru. Zaidi ya hayo, tulikuwa na kipindi kizuri cha shuhuda mbalimbali toka miongoni mwetu ambazo nyingi zilitugusa, kutufundisha na kututia moyo kuwa, hata katika magumu tunayopitia, bado sisi ni washindi.
Katika Somo la Biblia, Mchg. Osward Ndelwa alitupitisha katika tafakari ya neno la Mungu juu ya upatanisho. Katika tafakari hii ya siku mbili, tulitafakari maana ya upatanisho kiafrika na maana ya upatanisho wa kibiblia. Tuliona kuwa, upatanisho kiafrika ulihusisha watu wa rika fulani kusimama kama wapatanishi kwa wale waliokoseana au kwenda kinyume na matakwa ya jamii husika. Upatanisho huo uliendana na kutoa vitu mbalimbali kama vile wanyama, pombe na vingine vingi, kama ishara na sadaka ya upatanisho.
Tofauti na upatanisho wa kiafrika, upatanisho wa kibiblia, ni ule wa Mungu mwenyewe ambaye alimtoa mwana wake wa pekee Yesu Kristo, ili afe kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa kufanya hivyo, alijitambulisha kwa wanadamu kama fidia ya wengi. Huu ndio upatanisho unaoleta kuwajibika. Wajibu wa kuwaleta watu kwa Yesu kwa njia ya kushuhudia, kupeleka injili kwa njia mbalimbali ikiwemo hii ya maandiko ya neno la Mungu.
Pamoja na mafundisho na majadiliano mbalimbali, kama wafanyakazi, tulipata nafasi nzuri ya kushiriki kujifunza kupitia vitabu na mafundisho mbalimbali yanayotumika kwa rika tofauti tofauti. Kwa mfano, tulikuwa na kipindi kizuri cha kujifunza kuhusu ”Masomo Bunifu ya Biblia”, ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto wa shule ya Jumapili. Tulipata nafasi nzuri ya kujua umuhimu wa masomo haya na namna ambavyo yanaweza kutumika kuwafundishia watoto wa rika mbalimbali. Kila kituo kilipata nafasi ya kuelezea vitabu viwili vya changuo lao kwa undani, kama sehemu ya mafunzo yanayohamasisha msambaza maandiko kujua kile ambacho anataka wateja wake wakijue.
Kama wafanyakazi, hii pia ilikuwa ni fursa nzuri kutafakari kwa kina juu ya maendeleo ya kazi zetu na changamoto mbalimbali kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi zetu za kila siku. Moja ya vitu vilivyogusa wafanyakazi ni kutambuliwa kwa mchango wa wafanyakazi wenzetu ambao wamefanya kazi na Soma Biblia kwa muda mrefu. Kati yao wapo waliofanya kazi kwa miaka 10-30. Kutambuliwa kwao kuliambatana na cheti pamoja na zawadi maalumu toka uongozi wa juu wa Soma Biblia. Hii liliwavutia na kuwatia moyo wafanyakazi wengine, na kuona kuwa kumbe mchango wanaoutoa unaonekana na unathaminiwa.
Katika kusambaza maandiko, kulikuwa na shindano dogo la kutathmini ni kituo gani kilifanya vizuri zaidi kuliko vituo vingine, ambapo Soma Biblia Mwanza waliibuka washindi wa jumla, na kupewa Kikombe cha Ushindi. Hizi zote ni motisha kwa wafanyakazi, kuwaonyesha kuwa, kazi yao si bure, inaonekana na inathaminiwa. Sifa, heshima na utukufu ni kwa Mungu wetu, aliyetuwezesha kufanya haya yote.