RIZIKI TOLEO LA 04/2021
Cathbert Msemo
Maisha ni ubatili ikiwa hatutashika utukufu wa msalaba, kuuthamini kama hazina muhimu, na kushikamana nao kama kitu cha thamani sana ambacho gharama yake huwezi kuilinganisha na kitu chochote duniani. Japo awali msalaba ulionekana kama kitu cha kipumbavu kwa mwanadamu, lakini Mungu alikigeuza kuwa kitu cha thamani. Kile ambacho hapo kwanza kilionekana kitu cha kipumbavu, Mungu alikifanya cha maana kwa mwanadamu.
Juu ya msalaba tunaona wokovu; juu ya msalaba tunaona maisha mapya; na juu ya msalaba tunaona ulinzi dhidi ya adui zetu, na tunashuhudia jinsi fahamu zetu zinavyotiwa nguvu na kupata furaha na utoshelevu wa kiroho.
Katika toleo hili la Riziki tunajadili kuhusu nguvu ya msalaba. Ni mahali ambapo Yesu Kristo alitundikwa yapata miaka elfu mbili iliyopita, lakini tukio lile lilisababisha mabadiliko makubwa sana katika ulimwengu. Ni tukio hili ambalo lilirudisha uhusiano wa Mungu na mwanadamu. Yeye ambaye hapo kwanza alikuwa amegombana na Baba yake wa mbinguni, sasa amerudishiwa nafasi yake kama mtoto na mrithi pamoja na Kristo.
Pia utakutana na mtu mmoja ambaye hapo kwanza aliliudhi kanisa, lakini baada ya kukutana na Yesu maisha yake yalibadilika kabisa, hata kukiri waziwazi kuwa haoni fahari juu ya kitu chochote isipokuwa msalaba wa Yesu Kristo.
Vilevile utapata kusoma makala mbalimbali zitakazokusaidia, kukujenga na kukusogeza karibu na Mungu. “Kwa maana neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaokolewa ni nguvu ya Mungu” (1 Kor 1:18).
Bonyeza hapa kusoma bure
Pia unaweza kujisajili na kupokea matoleo yote manne ya mwaka kwa njia ya posta. Bonyeza HAPA kujisajili