SOMABIBLIA SEMINA 2016
Anne Gihlemoen
Kila mwaka Somabiblia huwakutanisha wafanyakazi wake kutoka matawi yote hapa Tanzania kwenye semina yenye lengo la kuwajenga katika huduma bora inayoendana na malengo ya shirika, lakini pia kufundishana maswala mengine ya kiimani, Kijamii na maisha na hasa yenye kuboresha mahitaji yao kama wafanyakazi.
Mwaka huu wa 2016, semina imefanyika mkoani Arusha katika kituo cha Canossa spiritually center, tarehe 09 hadi 11 mwezi wa sita, ikiwa na mafundisho mbali mbali na kumalizika kwa safari ya kutembelea Mbuga ya wanyama Ngorongoro.
Soma Biblia inamatawi matano, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Iringa na Mbeya. Wafanyakazi na viongozi wote huanza kwa safari kutoka kwenye matawi yote hadi eneo la semina na baada ya kuwasili semina huanza kwa kupata chakula pamoja, sala, Neno la Biblia, nyimbo na kufahamiana, na mengineyo.
Mkurugenzi wa SomaBiblia Odd Geir Norland ndie aliyefungua semina kwa nyimbo kutoka Tenzi za rohoni na. 10 ‘Usinipite Mwokozi’, maombi na Neno la Biblia. Hakika ilipendeza sana Zaburi ile aliyofungua nayo, Zab. 103 “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake Takatifu...”
Ujumbe wa kwanza na wakuvutia ulitoka kwa Mwanasheria na mtumishi wa Mungu, Willium E. Kivuyo, wenye kicha, “Usiwe muuzaji na msambazaji tuu wa Biblia na vitabu vya kikristo – uwemsomaji na mtendaji wa Neno.
Bwana Omari, Afisa ushirika halmashauri ya jiji la Arusha alieleza kuhusu SACCOS yaani Saving and credit co-operative Society. Asasi ya kifedha inayoundwa na wananchi au vikundi vilivyoamua kwa hiyari yao wenyewe kukusanya fedha kidogo kidogo kwa lengo la kujiwekea akiba na baadae kukopeshana.
Kwa upande mwingine mafunzo yaliyobeba uelewa juu ya mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF ulikuwa na majadiliano mazuri na kuwawezesha wafanyakazi kuamua kujiunga na mfuko huu utakao watibu wao na wategemezi watano katika vituo mbalimbali vya afya na hospitali nchini.
Vilevile kama ilivyo kazi kubwa ya Somabiblia kusambaza na kuuza Biblia na vitabu vya kikristo, kulikuwa na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuwafikia wateja na kuwapatia huduma kamili. Na pia kutoa shuhuda mbalimbali jinsi Mungu anavyowapigania katika maisha yao na katika kazi.
Mwisho wa semina ilikuwa safari ya kutembelea mbuga ya wanyama, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, huko kunamazingira na wanyama wazuri wenye kuuthibitisha uumbaji wa Mungu ulivyo mkuu na waajabu. Kweli wote walifurahi, kujifunza na kuwa na wasaa mmoja kama marafiki na wafanyakazi ndani ya shirika.
“Tusisahau fadhili zake Bwana, Daudi alihitaji na mimi ninahitaji, je wewe unahitaji?” Odd Geir Norland, Mkurugenzi SomaBiblia.