RIZIKI toleo la 01/2021 'Utusamehe makosa yetu' linapatikana
Cathbert Msemo
Nguvu ya msamaha
Miezi kadhaa iliyopita niliona katika taarifa ya habari nchini Marekani jambo lililonishangaza sana. Ilikuwa ni mwanamke mmoja afisa wa polisi ambaye alimwua mumewe katika mji wa Dallas. Wakati alipotangaziwa hukumu yake ya miaka kumi jela, mdogo wake marehemu alikuwepo mahakamani. Alimwomba hakimu dakika chache aongee na wifi yake. Katika hali ya upendo na huruma ya hali ya juu, alimwangalia akimwambia, “Kama kweli unaomba msamaha toka ndani ya moyo wako, naweza kuzungumza kwa niaba ya kaka yangu kwamba umesamehewa kabisa. … Nadhani jambo ambalo linaweza kumfurahisha kaka yangu ni wewe kumpa Yesu maisha yako. Nakupenda kama mke wa kaka yangu ambaye hayupo duniani. Sikuombei baya lolote likupate, bali umpate Yesu ndani yako.”
Msamaha sio jambo rahisi, lakini ndivyo Yesu alivyotufundisha. Siku moja Petro alimwuliza Yesu, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini” (Mt 18:21-22).
Ufafanuzi wa Sala ya Bwana unaendelea katika toleo hili la Riziki. Tumefikia sehemu ya tatu, Utusamehe makosa yetu, kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea. Msamaha ni jambo lenye nguvu sana. Tunapenda sana msamaha, lakini mara nyingi tunapotakiwa kukiri makosa yetu au kuwasamehe waliotukosea, tunaliona kuwa jambo gumu. Tunapenda kupokea msamaha lakini hatupendi kuutoa.
Utakutana na baba mmoja ambaye alimsamehe mwanawe aliyetapanya mali zote alizokabidhiwa. Habari hii itaweza kukusaidia kuishi kama Yesu alivyotufundisha katika Sala ya Bwana. Pia kuna makala nyingine zenye mafundisho mazuri ya kukujenga.