Twende toleo la 1/2025 - 'Linapatikana'
Cathbert Msemo
“Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima”
MPENDWA MSOMAJI
Hapo zamani kijijini kwetu kulikuwa na miti mingi mikubwa pamoja na migomba na vichaka vidogo vidogo. Hapakuwa na maeneo ya wazi. Tena nyumba zilikuwa chache na hapakuwa na umeme.
Wakati wa usiku giza lilikuwa nene kila mahali kiasi cha kushindwa kutembea popote bila usaidizi wa mwanga. Hivyo tuliwasha taa au tochi na kutembea ikituongoza njiani tusijikwae na kuanguka. Tuliishi sehemu za milimani. Hivyo ukitazama nje usiku uliona karibu kila mahali penye njia taa zikimulika na watu kutembea.
Taa hizi zilimulika eneo dogo tu la njia, na ulihitaji kuwa makini usiteleze na kuanguka katika mlima.
Ninakumbuka hali hii jinsi ilivyokuwa ngumu. Lakini imenisaidia kuelewa ninapotafakari tofauti kati ya nuru iliyoletwa na taa zetu, na Nuru ya ulimwengu. Biblia inatufundisha juu ya Nuru hii. Ni nuru kuu na ya ajabu, maana si mwanga tu unaotupa kuona bali nuru hii inatupa uzima.
Nikukaribishe kusoma toleo hili kuhusu Nuru ya Ulimwengu. Makala zote zinafafanua vizuri jambo hili. Usisahau michezo pamoja na katuni. Pia katika Sala ya Vijana utajifunza jinsi unavyoweza kuwa kielelezo kwa wengine ili nao wavutwe kumfuata Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Karibu tusome!
Nunua dukani Soma Biblia Dar es Salaam, Mbezi Luis, Arusha, Mbeya, Iringa, Mwanza,Dodoma